Arusha, Machi 24, 2026 – Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, leo amefungua rasmi Kongamano la 5 la Idhaa za Kiswahili Duniani katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Mhe. Abdulla ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwataja kama vinara wa mshikamano, maendeleo na mabalozi mahiri wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.
Aidha, amelitambua jukumu kubwa la Baraza la Kiswahili Tanzania na Baraza la Kiswahili Zanzibar kwa kuratibu kongamano hilo, akisisitiza kuwa Kiswahili ni nguzo ya utambulisho, mshikamano na diplomasia ya kikanda na kimataifa.
Katika hotuba yake, Mhe. Abdulla amewataka waandishi wa habari na wadau wa Kiswahili kutumia teknolojia za kisasa ili kufikisha lugha hiyo kwa hadhira pana zaidi duniani. Amesisitiza nafasi ya vijana katika mustakabali wa Kiswahili kupitia ubunifu wa kidijitali, ikiwemo maudhui ya mitandao ya kijamii, video za elimu na programu za simu.
Ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza Kiswahili kwa kuimarisha mafunzo ya ubunifu wa kidijitali, kuwezesha mitaji, kuboresha miundombinu ya TEHAMA na kushirikiana na sekta binafsi