Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kimeingia katika awamu mpya ya maboresho ya huduma kwa wateja wake baada ya Benki ya Azania kuzindua rasmi huduma za ATM ndani ya kituo hicho leo 16.03.2026, hatua inayolenga kurahisisha miamala kwa washiriki wa mikutano ya ndani na ya ya kimataifa.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa huduma hiyo , Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe, amesema uwepo wa huduma hiyo ni suluhisho la kimkakati katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za kifedha iliyokuwa ikiwakabili wadau na wageni wa kituo hicho.
“Biashara yetu kuu hapa AICC ni mikutano ya kimataifa na kitaifa. Uwepo wa ATM hii utatatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za kifedha na kurahisisha miamala kwa wageni wetu wanaotoka kila pembe ya dunia,” amesema Bi. Mwakatobe.
Vile vile, Bi. Mwakatobe ameupongeza uongozi wa benki hiyo kwa mwitikio wao wa haraka na ushirikiano uliowezesha huduma hiyo kuanza kutolewa. Aliongeza kuwa AICC itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha pande zote mbili zinanufaika kikamilifu na uwekezaji huo.
Uzinduzi huu ni sehemu ya jitihada za AICC kuendelea kuwa kituo bora cha mikutano barani Afrika kwa kutoa huduma jumuishi na rafiki kwa wateja na sekta ya mikutano.