Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kinga ya jamii ili kulinda ustawi wa Watanzania. Akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii leo, Februari 9, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Deus Clement Sangu, amesema kuwa “Kinga ya jamii ni haki ya msingi ya binadamu” inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Mhe. Sangu amebainisha kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta hii, ikilenga kuimarisha mifumo ya kisheria na kifedha ili kuwalinda wananchi dhidi ya changamoto kama magonjwa, ulemavu na ukosefu wa kipato.
“Ni wajibu wa wadau kutumia mkutano huu wa siku mbili kuibua mikakati thabiti itakayohakikisha kila mwananchi ananufaika na mifumo hii kwa tija,” alisema Mhe. Sangu.
Mkutano huo uliobeba kauli mbiu ya “Kinga ya Jamii kwa Wote Msingi wa Maendeleo”
umewakutanisha watunga sera na wadau wa maendeleo kwa lengo la kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuweka mwelekeo mpya wa kuwafikia wananchi wengi zaidi.